Mshambuliaji wa Mtibwa sugar, Musa Hassan 'Mgosi' amezifunga Simba, Yanga na Azam kwenye msimu uliopita.
Jumanne ya wiki hii, Mgosi alisaini mkataba wa kazi na klabu yake ya zamani ya Simba baada ya mkataba wake na Mtibwa kumalizika.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) bado halijafungua rasmi usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na ndio maana klabu zote nyingi zinawasainisha mikataba wachezaji wapya, huwa wanawapa mikataba ya kazi ambayo ni ya klabu na baadaye watasaini mikataba inayotambulika na TFF.
Chanzo cha habari kutoka Simba, kilisema kuwa Mgosi alisaini mkataba huo baada ya kufikia makubaliano na viongozi na hivyo atatangazwa rasmi pindi dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Kwa upande wa Mgosi wakati akihojiwa na chanzo hiki alisema: “Kilichofanyika ni mazungumzo tu ya usajili ambayo yamefikia pazuri, kama tutafikia makubaliano basi nitasaini na nitacheza Simba msimu ujao, hivyo ngoja tusubiri.”
Mpaka sasa Simba imemsajili mchezaji kutoka Mbeya City FC, Peter Malyanzi na kuwaongeza mikataba mipya wachezaji wake wa zamani Said Ndemla, Hassan Isihaka, Ibrahim Ajibu huku wengine kama William Lucian ‘Gallas’ na Abdallah Seseme pamoja na Ramadhan Singano wakiwa katika mazungumzo ya kuongezewa mikataba mipya.
0 comments :