Wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesikitishwa na kufanya vibaya kwa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars huku wakitaka makocha wazalendo wapewe nafasi ya kuinoa timu hiyo.
Katika maoni ya wabunge hao kwenye mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jana bungeni, wabunge hao wameeleza kuwa, hali ya michezo nchini ikiwamo soka, inasikitisha.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii licha ya kuipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, lakini ilieleza masikitiko yake kuhusu Taifa Stars.
"Hata hivyo, Kamati inasikitishwa na timu ya Taifa kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa. Hivyo, Kamati inaishauri Wizara kuendelea kuhamasisha wachezaji kujifunza zaidi ili siku nyingine waweze kupeperusha vizuri bendera ya Taifa," alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Manyovu, Albert Ntabaliba (CCM).
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu kuanzia kwenye ngumi, riadha, netiboli, mpira wa kikapu na kwa kiwango kikubwa kwenye mchezo wa soka. Hayo yalisemwa na Msemaji wa Kambi hiyo kwa wizara hiyo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema).
0 comments :