KAMA
hujawahi kupata fulsa ya kumuona na unasikia tu jina na mambo afanyao
uwanjani, huwezi kudhani kama anayetajwa ni mtu mwenye mwili usioendana
na mambo makubwa afanyayo ndani ya dimba.
Ni
kijana mdogo, mwembamba, mfupi, mwenye sura yenye haiba ya aibu wakati
mwingi na asiye na maneno mengi ya kuzungumza katika kadamnasi lakini
nyuma yake kuna vitu vingi vilivyojificha.
Huyu
ni winga machachari na mwenye kasi wa Dar Young Africans, Simon Msuva,
ambaye alijiunga na timu hiyo msimu uliopita akitokea Moro United ambayo sasa
ipo Ligi Daraja la Kwanza baada ya kushika daraja misimu miwili iliyopita ambayo
pia ina hali mbaya.
Msuva
anayefanana kiuchezaji na Mrisho Ngassa, anasifika kwa uwezo wa kupiga
chenga, kukimbia na mpira na kupiga krosi kali zenye madhara kwa timu
pinzani japokuwa kuna wakati hujisahau na kutaka kufunga mwenyewe hata
akiwa eneo gumu kufanya hivyo.
KUTOKA DANSA HADI SOKA
Msuva
kama ilivyo kwa vijana wengine wanaoweza kujaribu maisha kupitia fani
mbalimbali, mwaka 2004 hadi 2005, alikuwa akishiriki kucheza muziki
katika kundi la Tanzania House of Talent (THT) akiwa kama mwanafunzi wa
'kudansi'.
Lengo
la Msuva lilikuwa kutazama labda angeweza kufikia mafanikio ya maisha
yake kupitia muziki na siyo kwa kuimba wala kutunga nyimbo, bali kucheza
muziki na hii ni kutokana na kupenda zaidi muziki na kuwa na marafiki
wengi walio wanamuziki na zaidi wale wa kudansi.
“Nilidhani
kazi ya kucheza muziki ingeweza kunisaidia kunitoa na kufikia malengo
yangu, lakini mambo hayakuwa hivyo kwani baada ya muda mfupi tu nikiwa
najaribu kushiriki na rafiki zangu wa THT, nikaona kucheza muziki
kunaweza kunichukulia muda mwingi kabla ya kupata mafanikio katika
maisha,” anasema Msuva.
Baadhi
ya vijana ambao Msuva alikuwa akicheza nao muziki THT ni Msami na
Malenga ambao anadai walikuwa rafiki zake wa damu wakiwa katika kundi
hilo na wote walikuwa na malengo ya kufika mbali kupitia muziki.
AJIKITA UWANJANI
Kutokana na kuwa vipaji viwili na vyote akiamini kuvimudu vilivyo, Mwaka 2006, Msuva alijiunga na timu ya mchangani inayojihusisha na ukuzaji wa vipaji vya vijana wadogo ijulikanayo kwa jina la Wakati Ujao, ambayo aliichezea hadi mwaka 2007 alipojiunga na timu ya Academy.
Akicheza kama mshambuliaji wa kati na wakati mwingine winga, Msuva aliichezea Academy hadi mwaka 2008, alipojiunga na timu ya kukuza vipaji vya vijana ya Azam ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa.
Ndoto
zake za kucheza soka nusura zifikie ukingoni baada ya timu hiyo ya Azam
kuvunjika mwaka 2008 mwishoni, jambo lililomfanya Msuva kurejea katika
kituo cha Academy kuendelea kujifunza soka.
ANG’ARA COPA COCA COLA
Katika mashindano hayo, ambapo Msuva alifanya vizuri akiwa na kikosi cha Academy, mwaka 2009 na 2010, alichaguliwa kucheza michuano ya taifa ya vijana chini ya miaka 17
ya Copa Coca Cola, na kupata nafasi ya kuitwa katika timu ya taifa ya
vijana chini ya miaka 17.
Akiwa
na timu hiyo ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 maarufu kama
Serengeti Boys, Msuva alijiunga na vijana wenzake kuelekea katika mechi
ya timu hiyo iliyochezwa Sudan.
ATUA MORO UNITED
Baada
tu ya kurejea nchini Uwezo, juhudi na kufuata vyema maelekezo ya
mwalimu na kuweza kuwika dimbani kwa Msuva akiwa na Serengeti Boys,
kulimfanya kinda huyo kuonekana na kuvutiwa na Klabu ya Moro United,
waliomsajili katika kikosi chao cha vijana mwaka 2010.
Akiwa
Moro United, Msuva alifanya vizuri kiasi cha kuibuka mfungaji bora wa
michuano ya vijana wa timu za Ligi Kuu ya Bara maarufu kama Uhai Cup,
inayofanyika kila mwaka kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Baada
ya kuibuka mfungaji bora katika Kombe la Uhai, Msuva alipandishwa hadi
kikosi cha kwanza cha Moro United japokuwa hakuwa akipata nafasi mara
kwa mara.
ARUDI AZAM
Akiendelea
kufanya vizuri akiwa dimbani, Mwaka 2011, Msuva alihama Moro United na
kuerejea Azam ambako alipelekwa kikosi B huku akiwa na nafasi ya kucheza
Ligi Kuu ya Bara.
Hata hivyo, pamoja na kurejeshwa katika kikosi cha Azam, Msuva anakiri kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa vijana wa akiba, mpango wa baadaye wa timu hiyo hivyo hakuweza kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, pamoja na kurejeshwa katika kikosi cha Azam, Msuva anakiri kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa vijana wa akiba, mpango wa baadaye wa timu hiyo hivyo hakuweza kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Azam
walinisajili hadi katika ligi kuu, lakini hawakuweza kunichezesha mechi
za ligi kwa kuwa mimi nilikuwa mmoja wa wachezaji waliopanga kuwatumia
siku za baadaye baada ya kupata uzoefu zaidi.
“Lengo
lao lilikuwa mimi nianze kucheza kuanzia labda mwaka 2014, kwa kuwa
umri wangu uliruhusu kuweza kusubiri huku nikiendelea kupata uzoefu
kutoka kwa wachezaji wengine wa timu kubwa,” anasema Msuva.
Mwaka jana Msuva alirejea tena Moro United kabla ya kusajiliwa na Yanga mwaka huohuo.
ANAPENDA KUCHEZA NA TEGETE, ANAMKUBALI BARNABA THT
Huku
akisuasua, Msuva anasema anapenda zaidi kucheza sambamba na
mshambuliaji Jerry Tegete, japokuwa anapenda kucheza na washambuliaji
wote wa Yanga katika kikosi cha kwanza, sababu kubwa ikiwa ni ujanja wa
Tegete awapo katika lango la timu pinzani.
“Washambuliaji
wa Yanga wote naona ni wazuri kucheza nao, lakini Tegete ni mjanja
zaidi mnapokuwa mnashambulia kwa kuwa ana uwezo wa kucheza mipira
inayodharauliwa na adui zetu na pia kucheza mahala ambapo huamini kuwa
angeweza kucheza.
“Unaweza
kupiga mpira ukadhani (Tegete) hayupo eneo hilo, lakini ghafla unaweza
kumuona ameshafika na kuucheza mpira, japoa hana speed kali lakini ni
mjanja wa kujipozisheni tu. Pia ni mfungaji mzuri wa mabao ya vichwa,”
anasema Msuva.
Kwa
upande wa muziki, Msuva anamkubali zaidi Elius Barnaba ambaye naye ni
zao la THT kama alivyo yeye. Anapenda jinsi anavyojituma kimuziki
kutunga, kuimba na namna anavyoweza kuwasaidia wenzake.
“Namkubali
sana Barnaba maana anajituma ipasavyo katika muziki wake na kazi zake
nyingi ni nzuri na za kupendeza, yeye ni mfano mzuri kwa vijana wote
ambao tunatafuta maisha kupitia sanaa na utamaduni,” anasema Msuva.
HAJAWASAHAU WASHKAJI ZAKE THT
Tofauti
na mastaa wengine ambao husahau mahali walipotokea, Msuva mara kadhaa
amekuwa akiwatembelea rafiki zake wa THT ambao alishirikiana nao katika
kucheza muziki na hupiga nao stori kama kawaida.
“Siwezi
kusahau nilipotoka, mara nyingi huwa naenda THT na kuzungumza mambo
mbalimbali na rafiki zangu ambao wamebaki pale. Hakika ni kitu
ninachojivunia siku hadi siku na naamini wao ni sehemu ya mafanikio
yangu katika soka,” anasema Msuva.
Msuva
anasema, akiwa THT hukutana na kuzungumza na wasanii wote hata wale
ambao sasa hawapo kama Barnaba ambaye anakubali kazi zake na kupeana
changamoto mbalimbali za kimaisha.
HAPENDI MARAFIKI WANASOKA
Unaweza
kumuona ni mtu wa ajabu lakini ndivyo ilivyo hata kwa wanasoka wakubwa
duniani, Msuva hapendi kujenga urafiki mkubwa na wachezaji wenzake kwa
kuwa muda mwingi atakuwa akifikiria zaidi soka pekee na kupoteza mambo
mengine katika jamii.
“Niliwahi
kushauriwa na 'Kaka yangu' Mtemi Ramadhan, aliniambia kuwa kitu kimoja
kikubwa sana katika maisha ya soka, ni kwamba sipaswi kuwa na marafiki
wengi ambao ni wanasoka pekee ambao muda mwingi huzungumza lugha moja ya
soka tu.
“Kama
binadamu, napaswa kuwa na marafiki wanaojishughulisha na mambo mengine
ili tu niweze kupanua wigo wangu wa uelewa na mawazo. Nadhani ni ushauri
mzuri na naona unanijenga siku hadi siku na kunisaidia,” anasema Msuva.
“Mimi
bado ni kijana mdogo, Yanga ni timu kubwa na pia kuwa wachezaji
wenzangu wengu tu wakubwa na wazoefu kunizidi, sasa kuna vitu lazima
ukumbane navyo unapojiunga na timu kubwa kama hii lakini nashukuru Mungu
nimeweza kujiunga na timu kubwa kama hii na kucheza kikosi cha kwanza,”
anasema Msuva.
Anasema
wachezaji wakongwe na wale wa kimataifa wanaendelea kuwa kioo kwake kwa
maisha ya ndani na nje ya uwanja na mara kadhaa huwauliza kuhusu mambo
mbalimbali ya soka.
“Mwanzo
nilikuwa siamini kama nipo Yanga na wala nilikuwa siamini kuwa nacheza
na wachezaji maarufu, lakini sasa nipo nao na naishi nao vizuri na wao
ni washauri wazuri kwangu na naamini hadi kufikia hapa nilipo wao
wameshiriki kwa kiasi kikubwa sana kunisaidia kwa namna moja ama
nyingine,” anasema Msuva.
Mara
nyingi Msuva hupokea ushauri kutoka kwa kiungo Haruna Niyonzima, Hamis
Kiiza, Athuman Idd Chuji na wakongwe wengine wa Yanga.
SASA SI KAZI BURE
Mwanzo
wakati anaanza kupata nafasi kikosi cha kwanza cha Yanga, Msuva alikuwa
anachezeshwa kama winga nafasi anayoicheza hadi leo hii, lakini mara
nyingi alikuwa akikimbia na mpira muda mrefu huku akijaribuku kutaka
kufunga hata kama yupo ‘impossible angle’, lakini siku hizi kwa kiasi
kikubwa amebadilika, ambapo amekuwa akipiga krosi nyingi na zenye
malengo.
“Unajua
mimi wakati nasajiliwa Yanga kutoka Moro United, kule nilipotoka
nilikuwa nacheza kama mshambuliaji sasa Yanga nachezeshwa kama winga
hali inayonifanya niwe natamani zaidi kufunga kila ninapojisahau kuhusu
nafasi niichezayo.
“Lakini
kwa sasa namshukuru kocha ananielewa na sasa namimi nimemuelewa baada
ya kuniambia nisiwe mchoyo wa pasi, niwe nawapa wenzangu pasi mapema na
wala siharibu kama ilivyokuwa mwanzo. Nadhani sasa nacheza vizuri
tofauti na mwanzo,” anasema Msuva.
ANAVUTIWA NA RONALDO, DOMAYO LAKINI ANAIPENDA MAN UTD
Ronaldo |
Msuva
ni shabiki mkubwa wa mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na
kiungo wa Yanga, Frank Domayo. Anasema anampenda Ronaldo, kutokana na
aina ya uchezaji wake lakini Domayo ni zaidi ya mchezaji na rafiki
kwake.
Frank Domayo (kulia) |
“Domayo
ni rafiki yangu katika kikosi cha Yanga pia navutiwa na aina yake ya
uchezaji na pia huwa ananishauri mambo mbalimbali na hata mimi hufanya
hivyo kwake.
Ni mchezaji ambaye naamini atafika mbali katika soka la Tanzania,” anasema Msuva.
Ni mchezaji ambaye naamini atafika mbali katika soka la Tanzania,” anasema Msuva.
Wakati
akionyesha wazi mapenzi yake kwa Ronaldo, Msuva ni shabiki mkubwa wa
klabu ya Manchester United ya England na hilo haoni haya kulificha na
yupo kifua mbele kuitetea klabu hiyo yenye maskani yake katika jiji la
Manchester.
“Naipenda
Man United, ni timu nzuri yenye kila kitu cha kuiwezesha kutwaa mataji
mbalimbali ndani na nje ya England japokuwa tayari imeshatolewa katika
Ligi ya Mabingwa Ulaya,” anasema Msuva.
PIA NI KIONGOZI WA MITINDO YA KUSHANGILIA KATIKA KIKOSI CHA YANGA
Tazama
mechi yeyote ya Yanga kwa umakini, mara tu timu hiyo inapopata bao
wachezaji wote humwangalia Msuva na kumfuata huku wakimfuatisha kucheza
na yeye ndiye mbunifu wa mitindo yote ya uchezaji na hii inawezekana ni
kutokana na yeye kuwa mkali wa kudansi hapo awali.
“Tangu nilipokuwa Moro United, nilikuwa kinara wa kubuni mitindo ya kushangilia.
Hapo naweza kubadilisha kutoka mmoja hadi mwingine kulingana tu na mechi yenyewe.
Wachezaji wenzangu kabla ya mechi hunifuata na kuniuliza jinsi ya kushangilia mimi huwaelekeza nini cha kufanya,” anasema Msuva ambaye hana mke wala mtoto.
KWA TAARIFA YAKO…
Msuva
aliyezaliwa mwaka 1993, na kusoma shule ya msingi ya Lions iliyopo
Magomeni, Kinondoni jijini Dar es Salaam anapenda kuigiza sauti za
wanamuziki kama Ben Pol na Belle Nine wanaoimba muziki wa kizazi kipya
na pia hupenda sana kusikiliza nyimbo za wasanii hao.
Chipukizi
huyu anapenda kunyoa nywele zake kwa mtindo wa kiduku, lakini hivi
karibuni uongozi wa Yanga ulimpiga mkwara na kumshauri kuondoa staili
hiyo ama kunyoa kabisa ili asiweze kuvimba kichwa.
“Nimeambiwa
ninyoe nywele zangu, sina tatizo nimezinyoa lakini naamini mimi ni
mkubwa na naweza kujiongoza katika mambo mbalimbali bila ya kupotea kama
uongozi unavyodhani,” anasema Msuva ambaye bado anaishi na wazazi wake,
huko maeneo ya Kimara jijini Dar.
0 comments :