Tangaza hapa

e

Featured Posts

Monday, 23 March 2015

Suarez aiongoza Barcelona kuiua Madrid Camp Nou

Unknown     10:30    


 Barcelona walipanua mwanya uongozini La Liga kutoka alama moja hadi alama nne baada ya kuwachapa mahasimu wao wa jadi Real Madrid 2-1 kwenye mechi kali ya El Clasico iliyochezewa uwanjani Nou Camp Jumapili.

Mechi hiyo ilijaa kadi, Pepe akiwa wa kwanza kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 21 kwa kumchezea visivyo Luis Suarez, lakini raia huyo wa Uruguay alimfuata upesi Pepe kwenye buku la refa baada ya kumchezea visivyo Pepe dakika ya 27.
Wengine waliolishwa kadi ni Jordi Alba, Javier Mascherano na Andres Iniesta upande wa Barcelona, na Carvajal, Sergio Ramos, Luka Modric, Isco na Cristiano Ronaldo upande wa Real Madrid.
Barca waliona lango kwanza wakifungiwa na Jeremy Mathieu kwa kichwa dakika ya 19. Difenda huyo wa Ufaransa alifikia frikiki iliyochapwa na mchawi wa mabao Lionel Messi na akamzidi ujanja mlinzi wa Real Sergio Ramos na kufunga, likiwa bao lake la kwanza kufungia Barca katika La liga.
Cristiano Ronaldo hata hivyo alisawazishia Real dakika ya 31, kwa bao lake la 15 la El Clasico, baada ya kupokea pasi safi ya kisigino kutoka kwa Karim Benzema.
Dakika ya 40, Real awalidhani wamepata, baada ya Gareth Bale kutumbukizwa mpira wavuni baada ya kupokea mpira kutoka kwa Ronaldo lakini refa akasema alikuwa ameotea.
Pande zote mbili zilielekea mapumzikoni zikiwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili Luis Suarez, aliyenunuliwa kutoka Liverpool mwaka jana, aliwarejesha Barca mbele dakika ya 56 akipokea mpira wa mbali kutoka kwa Dani Alves na kisha kumbwaga kipa Iker Casillas, likiwa ni bao lake la sita katika mechi saba za La Liga alizocheza karibuni zaidi.
Timu zote mbili zilizidi kushambulia, kipa wa Barca Claudio Bravo akilazimika kufanya kazi ya ziada kuzima kombora la Benzema lililokuwa likielekea wavuni, Casillas naye akilazimika kutumia ustadi wake kuzima Messi dakika za mwisho za mechi.
Barca wamekuwa na kipindi kizuri wakishinda mechi tisa kati ya 10 walizocheza kabla ya El Clasico hiyo, kinyume na Real ambao wamekuwa taabani kwa kucheza vibaya, hata katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambako nusura wabanduliwe na Schalke 04 ya Ujerumani mechi ya hatua ya 16 bora. Hali hiyo imemuwekea presha meneja wao Mwitaliano Carlo Ancelotti.
Barcelona kwa sasa wana alama 68, wakifuatwa na Real walio na alama 64, Valencia wakiwa wa tatu na alama 60. Mabingwa watetezi Atletico Madrid wamo nambari nne na alama 59.

0 comments :

Top headlines

© 2011-2014 MICHEZONI. Designed by Alfred Meshack Bloggertheme9. Powered by Blogger.