Msimu wa 2015/2016 Ligi Kuu soka Tanzania Bara, unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi ya wiki hii kwa michezo saba kuchezwa katika viwanja tofauti nchini.
Ratiba ya mechi za ufunguzi ilitumwa jana mchana na Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguito na kueleza kuwa Ndanda FC ya Mtwara watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Nagwanda Sijaona, Mtwara.
Huku ‘Wana kimanumanu’ African Sports watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na ‘Wana Lizombe’ Majimaji wakiwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Majimaji, Songea.
Azam FC watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons katika Uwanja wa Chamazi Complex, Stand United FC ‘Chama la wana’ watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kambarage Shinyanga, Toto Africans watawakaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City watacheza na Kagera Sugar katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Jumapili Ligi Kuu itaendelea kwa mchezo mmoja tu utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga SC watawakaribisha ‘Wagosi wa kaya’ Coastal Union.
Katika hatua nyingine klabu ya Kagera Sugar ya Kagera itatumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora kwa mechi zake za nyumbani dhidi ya Toto Africans (Sept 26), JKT Ruvu (Sept 30), Tanzania Prisons (Oct 4) na Yanga (Oct 31).
Mabadiliko hayo yamefanyika kupisha shughuli ya uwekaji nyasi bandia inayoendelea kwenye uwanja wao wa Kaitaba, Bukoba unaofanywa na wataalamu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
0 comments :